Muhibu Huyu (Swahili Poem)

Njiwa upelekaye salamu
subira leo imeniisha.
Kabla hujaleta jibu
namfuata mpokea salamu.

Si barua wala ujumbe
hoja yangu nimtie machoni.
Muhibu huyu ameninata
kama asali changa ya Singida.

Sura yake imenipagaza
maruhani wapigwa butwaa.
Kaka huyu ananipa shauku
madaha ya Tanga yameniisha.

Mwendo wake maridadi
bingwa wa utanashati.
Nazaa ya kike imeniisha
utawa leo kwangu adimu.

Maulana siombi busara
kunusurika na penzi hili.
Dhamiri yangu kukwatua
ushawishi wa jibli yake.

Njiwa leo baki tunduni
juhudi yako nashukuru.
Hedaya ya sauti yake
tamati ya ashiki zangu.

©Gloria D. Gonsalves

Recent Comments

  • George Kyomushula
    August 9, 2014 - 11:03 pm · Reply

    EWE NJIWA LEO HII HU WAPI ?

    Njiwa leo hii hu wapi ?/ Majibu ya ujumbe mbona sipati?/
    Penzi langu kwake ni la dhati/Ujumbe kuuleta hautaki ?/
    Njoo uipoze yangu nafsi / Ili nami nipate kutamaraki /
    Njiwa leo hii hu wapi ?/ Mbona majibu ya ujumbe sipati ? /

    Tuwaache wakina nenga / Wenye husda za kuchonga ngenga /
    Pasi na shaka nitamuita mshenga /baina yetu aje akipulize kipyenga /
    Mungu bariki nisije kukutenda /kwa dhati nimenuai penzi kulijenga /
    Njiwa leo hii hu wapi /mbona majibu ya ujumbe sipati ? /

    Binti huyu mwenye haiba /hakika nitajaribu kumuiba /
    Mafunzo nishayapata kwa ngariba / nikiwa naye nitawakwepa maswaiba /
    hasa wenye ufitini wa kiakida/ watakuja tu kutuletea shida /
    Njiwa leo hii huwapi / mbona majibu ya ujumbe sipati ?/

    Sauti yake maridadi / kuisikiza napataje midadi /
    njiwa fanikisha miadi /ili twende kwenye fukwe ya Mikadi /
    nikapate mabusu yasiyo na idadi / hata ikinyesha mvua yenye radi /
    Njiwa leo hii hi wapi / majibu ya ujumbe mbona sipati /

    Njiwa embu kwanza acha uzembe / usipokuja nitaenda lazwa Milembe /
    majibu nipe yanitoe wenge / sitaki kuwa mshika mapembe kwa utam wa kula tende /
    moyo uje uchanwe kwa kiwembe / kwa hadaa tu ya peremende /
    Njiwa leo hii huwapi /majibu ya ujumbe mbona sipati ?/

    ©Kyomushula

  • Eric
    November 5, 2014 - 11:24 pm · Reply

    Hahahahaa… “….kama asali changa ya Singida.” kwa kweli shairi hili nimelipenda sana hasa mstari huu maana umenikumbusha nyumbani. Hahahaha…

Leave a Comment