Skip to main content

“…Tumejipanga vyema kuilinda nchi hii… Kwa hiyo hakutakuwa na nywinywi wala nywinywinywi…”– Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Septemba 2025

“…Na sisi tumejipanga wanajeshi kuilinda nchi na kuwalinda wananchi…Yeyote ajitokeze alete fyefyefye au fyofyofyo sisi tutamletea fyokofyoko…” – Afande kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Oktoba 2025

Mimi nitakuwa huku
hata unipe zako buku.

Wewe utakuwa kule
hata iamke misukule.

Lugha za majigambo
zimetawala mitambo.

Wakuu mbona viziwi
kwani mnaishi Malawi?

Uovu si jambo takatifu
si biblia wala msahafu.

Hasira za kuvumiliana
moto haukuanza jana.

Hakuna mbumbumbu
hoja mnazipa kabumbu.

Miundombiu ina uhaba
kandanda itajaza vibaba?

Ulafi ukikenua mapengo
kijacho ni fimbo mpingo.

Kusingizia wa diaspora
tunaona mnavyotupora.

Tukipuuzia zenu siasa
walafi wanajaza visasa.

Iwe nchini au ughaibuni
zinachosha zenu rubuni.

Ona maskini nchi tajiri
watunza misingi si hariri.

Mnatuletea mafarakano
kuzuga na yenu mitano.

© Gloria D. Gonsalves, 2025

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.