Skip to main content
Picha kwa hisani ya mwandishi

Misiba na harusi ni desturi zetu, wakuu sikilizeni wananchi.
Kishujaa tuwaage wafu wetu, mgawanyo tusiupe kipaumbele.
Iteni viongozi wetu wa jadi, iteni viongozi wetu wa dini.

Damu zimemwagika, taifa letu linahitaji kuweka matanga.
Unyenyekevu sio dhambi, wakubwa na wadogo wote ni miili.
Iteni vijana na wazee, iteni manguli waliobobea maziko.

Wengi tumebeba mawe, kuyatua hatuwezi bila maagano.
Hata makazini tuna jadi, kwenda mazikoni hakupewi maswali.
Iteni wale waliowatenda, iteni na wale mliowatenda.

Bendera zetu zipepee nusu, ili turejee kuzipeperusha nzima.
Uchovu wa moyo tunao sote, tupeane nafasi ya kuiponyesha.
Iteni waliotutangulia, iteni wahenga kutoka ardhini mwetu.

Watanzania ni wakimya, watanzania hao hao ni watemi.
Damu za Kinjekitile na Mkwawa, ujasiri kwetu ni dhahiri.
Iteni watemi wetu waliolala, iteni watemi wetu walio hai.

Maombi makuu mmeshayasikia, wasikilizeni vijana wetu.
Wakubwa mnazo busara, ila chachu ya vijana hutekelezesha.
Iteni watoto wetu kwa upole, iteni vijana wetu kwa heshima.

Uchawi na uchawa tuutupe, upendo na mshikamano tuweke.
Nchi yetu sio choo, tugange yajayo kwa jadi yetu ya kioo.
Iteni wana wenu wanadiaspora, iteni wana wenu wakimbizi.

Sala na swala zishamiri, mashehe na mapadri wakituongoza.
Muungano una sababu zake kuu, tusiwe wepesi wa hasira.
Iteni wale wote wa bara, iteni pia na wenzetu wa visiwani.

*Napokea masahihisho ya kiuhariri

2 Comments

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.