Skip to main content

“Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2024 fedha zinazotumwa na Diaspora kuja nyumbani ni shilingi 2,116,188,355,632.06 ukilinganisha na shilingi 2,045,855,200,000 kwa kipindi cha mwaka 2023. Kiasi hicho kina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya familia zao, kusaidia uwekezaji na kuchangia ukuaji wa sekta ya fedha nchini.” – Mhe. Waziri Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Serikali inatambua nafasi muhimu ya diaspora. Ndiyo maana tumekamilisha mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje inayojumuisha masuala ya diaspora, tumeanzisha mfumo wa kidijitali wa usajili wa diaspora, tumepitisha hadhi maalum kwa Watanzania wasio raia, na kuanzisha vitengo mahsusi serikalini vya kushughulikia masuala yao.” – Mhe. Chumi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Aprili 2025.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Wizara iendelee kuangalia namna ya kuimarisha diaspora katika kuchangia uchumi wa Tanzania. Nchi zinazoendelea zilizo nyingi zinategemea sana fedha ya kigeni kutokana na diaspora. Tunapoangalia ushiriki wa diaspora katika uchumi wetu, napendekeza Wizara iweke utaratibu wa vijana wetu kupanua ajira ya nchi za nje. Kutokana na changamoto za ajira ni bora pia kuangalia soko la ajira la nchi za nje.” – Hon. Oran Manase Njeza, Mbeya Vijijini, Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

“Diaspora ni rasilimali muhimu katika kuimarisha uchumi wa Afrika.” – Mhe. January Makamba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), hotuba ya Ufunguzi wa Kongamano la Nne la Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora), lililofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff Mjini Zanzibar Augusti 2017.

Mama Bongo jamani shikamoo.
Pole na changamoto za utekaji.
Naelewa, mimi huteka sana pia.
Ndio Mto Pangani upo karibu.
Nateka maji tangu nikiwa mtoto.
Unakiona kichwa kilivyo bapa?
Sihitaji tena kata ya kubebea ndoo.
Eti una jamaa yeyote kule Ulaya?
Huyo ndugu yako anaitwa Diaspora?
Ni mwanao wa kwanza au wa kambo?
Kumbe unaye mtoto anaishi ng’ambo.
Kifungua mimba mpe majukumu.
Wajibu wake ni kutunufaisha sote.
Mwambie rasilimali zimeshikiliwa.
Mali asili zako ni za wakubwa tu.
Hapana, wakubwa sio kama yeye.
Yeye afanye juu chini afidie uchumi.
Huko majuu si anachuma pesa sana.
Yaani yule usipomtumia basi tena.
Akikupigia simu orodhesha shida zetu.
Ndiyo mueleze shida hata za majirani.
Yule ni mti wetu unaopukutisha dola.
Akitaka kuja nyumbani mlipishe visa.
Akitua na vizawadi mtoze ushuru.
Kumpa urithi yeye wala usithubutu.
Akijaribu kurudi nyumbani mbane.
Hata ndugu zake wasimwamini sana.
Chochea wivu baina yake na ndugu.
Diaspora akufidie pale unapofisadiwa.
Usimwamini kuhusu kujikomboa.
Mwambie haki ni mambo ya huko.
Sisi maadam tuna amani hayamhusu.
Tena mnyime kabisa na uraia pacha.
Wewe toa ahadi lakini jivute kuzitimiza.
Msifie sana wakati wa bunge la bajeti.
Hakikisha unatamka kiwango anachochangia.
Mfumbe macho na takwimu za kimataifa.
Shida si aonekane wa maana ughaibuni?
Ona gazeti la National Geographic Traveller (UK).
Leo umekolea waridi kwenye kava lao.
Atapostiposti tu mtandaoni ili ajisikie.
Kila mwaka mpe tumaini la hadhi maalum.
Akisafiri kurudi ng’ambo kaza moyo usilie.
Wala usichukue hatua wakimwibia airport.
Akinai majukumu? Huwajui vifungua mimba?
Akikataa mtishie kwamba amekukana.
Ana upendo sana yule kitamgusa moyo.
Ila apende asipende majukumu atayabeba.
Wajibu wake ni kukusaidia sio kujisaidia.
Sasa utaandamana kwenda kupiga kura?

© Gloria D. Gonsalves, 2025

4 Comments

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.