Shairi (Poem): Mama Ni Hifadhi Ya Mwangaza

Mishumaa miwili iliwaka kwa mwangaza mkubwa.
Nuru yao ilisafiri kila kona ya nchi hadi magharibi.
Mwangaza huo haukuruhusu kamwe kivuli cha kuingiliwa.
Wenye nafasi na wasio nafasi kila mmoja aling’ara.

Safari ya maendeleo ilikuwa kasi kama moshi wa volkano.
Lakini jioni moja upepo wa ghafla ulizima mshumaa mmoja.
Huzuni, vilio, na simanzi vilitawala ndani na nje ya mipaka.
Sasa itakuwaje kwani mwangaza wa njia yetu umepungua?

Mshumaa uliobaki haukuyumba wala kutikisika kwa woga.
Ulibeba nia, matamanio, na pia ahadi za mishumaa yote miwili.
Kuzimika kwa mmoja haikuwa rahisi kusitiri na kukinga kiza.
Alhamdullilahi mwenye heshima ya mama ni hifadhi ya mwangaza.

Safari bado ndefu na mwangaza wa maendeleo ndiye mkombozi.
Basi na heri ikawe naye mama jemedari mshumaa wetu.
Baraka za waliomtangulia zisafishe mawimbi ya uchokozi njiani.
Nasi wapenda amani tumkinge kwa uvumba wa kazi na heshima.

* Kumbukumbu ya kuapishwa kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hasani, raisi wa kwanza mwanamke Tanzania (marking the inauguration of Her Excellency Samia Suluhu Hasani, the first female president of Tanzania).

Leave a Comment